About us
Lengo la Tovuti
Lengo la tovuti hii ni kuelimisha na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali pamoja na uwekezaji unaofanyika katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Aidha, tovuti hii inalenga kutoa taarifa halisi za ushiriki wa watanzania mathalani kupitia ajira, ununuzi wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa makampuni ya kitanzania, mafunzo na uhaulishaji wa ujuzi na teknolojia. Fursa mbalimbali zilizopo katika miradi hii zitaoneshwa katika tovuti hii ili kuhakikisha zinawafikia watanzania.
Msimamizi wa Tovuti
Tovuti hii inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), chini ya uangalizi wa kiteknolojia wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA).
Miradi ya Kimkakati ni nini?
Ni miradi mikubwa yenye vipaumbele inayotekelezwa na Serikali ambayo inalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania (Local Content) katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Miradi hii iwe ni ile yenye uwezo wa kutengeneza ajira kwa nguvu kazi ya ndani, na utoaji wa huduma za ndani, mfano wa miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), mradi wa barabara ya juu la Mfugale (Mfugale flyover) ambayo imekamilika hivi karibuni, barabara ya juu ya Ubungo (Ubungo interchange), ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha “standard gauge”,ujenzi wa daraja na barabara salender,ujenzi wa zahanati na vituo vya afya nchini.
Miradi ya Uwekezaji
Hii ni miradi ya uwekezaji inayohusisha wawekezaji wakubwa kutoka nje na ndani ya nchi inayolenga kuongeza thamani na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Lengo la Miradi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza miradi ya kimkakati kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya ukuaji wa kiuchumi kwa Taifa la Tanzania, ambayo inatarajiwa kuipeleka nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025. Miradi hii inasimamiwa na kutekelezwa na wizara pamoja na taasisi za Serikali na sekta binafsi. Uwepo wa miradi hii unachangia kukuza na kutoa fursa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kutoa ajira, kuwezesha biashara (ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani) kuwezesha urithishaji wa ujuzi na teknolojia kwa watanzania kutoka kwa wataalam wa kigeni wenye fani na ujuzi adimu na kukuza shughuli za kuchumi kwa jamii ya watanzania .
Utekelezaji wa dhana ya Ushiriki wa Watanzania (Local Content)
Utekelezaji wa masuala ya local content nchini Tanzania ni mtambuka hivyo unaogusa wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi. Miongoni mwa wadau hao ni pamoja na sekta ya umma (kupitia Wizara, Idara na Wakala wa Serikali), sekta binafsi (kupitia wawekezaji, wakandarasi, n.k).
Uratibu wa Ushiriki wa Watanzania katika Uwekezaji
Masuala ya local content ni mtambuka yanayoweka hitaji la umuhimu wa uratibu ili kuwezesha, upangaji wa mipango upatikanaji na upimaji wa taarifa za utekelezaji za ushiriki wa wananchi na makampuni ya watanzania katika miradi ya uwekezaji na ile ya kimkakati. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ina jukumu la kuratibu, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa masuala ya local content katika ngazi ya kitaifa kupitia sekta zote za vipaumbele kwenye kuzingatia masuala mbalimbali kama vile:-
- Upatikanaji wa ajira na uendelezaji wa nguvukazi ya wananchi wa Tanzania
- Mpango wa urithishaji ujuzi na teknolojia
- Kuhakikisha kunakuwepo na ubia kati ya makampuni ya Tanzania na wawekezaji ili thamani ya ziada iweze kubaki nchinina Taifa kunufaika na fursa hizo
- Uendelezaji wa watoa huduma wa kitanzania na ununuzi wa bidhaa/malighafi zilizopo nchini
- Ushiriki wa jamii n.k
Serikali ina jumla ya waratibu 557 wa local content amabao wako kwenye ngazi ya wizara na taasisi umma. vilevile waratibu 185 kutoka ngazi ya halmashauri ya wilaya.
sekta za kipaumbele kwenye local content ni pamoja na
- Madini, na Gesi Asilia
- Nishati
- Ujenzi
- Sayansi,Teknolojia na Elimu
- Utalii
- Manunuzi ya umma
- Kilimo,
- Fedha na Bima
- Viwanda
Uratibu unaofanyika unawezesha Serikali kutambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau hali inayoongeza chachu kwa Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji yanazing’atiwa katika hatua za awali, kabla, wakati na baada ya utekelezaji na upimaji wa masuala ya local content. Uratibu unawezesha kuishauri Serikali kwenye mambo mbalimbali ambayo huleta faida za ustawi na maendeleo ya Taifa. Kuwepo kwa uratibu kumesaidia kuongeza ufahamu wa hali halisi, fursa, changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa masuala ya local content katika sekta mbalimbali za kiuchumi.