Manunuzi

Manunuzi ya umma yana umuhimu mkubwa katika uchumi wowote kwani yanaweza kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi, utoaji wa huduma za umma na ukuaji wa sekta binafsi. Nchini Tanzania sheria inayosimamia Manunuzi ya Umma imepitia hatua mbalimbali kubwa za maboresho tangu ilipoasisiwa mwaka 2001. Mwaka 2004 Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA) 2001 ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2004 ambapoikawezesha Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuanzishwa. Mnamo mwaka 2016 Sheria hiyo ilirekebishwa ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na dhamana ya pesa. Pia marekebisho ya 2016 yamelenga kuingizwa kwa makampuni ya ndani na wataalamu katika mikataba ya ushauri, matumizi ya wataalam wa ndani wa bidhaa, kazi na mikataba isiyo ya huduma za ushauri, upendeleo kwa bidhaa za ndani na ujenzi wa uwezo wa makampuni ya ndani. Ililenga pia kuongeza ushiriki wa vikundi maalum (wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu) katika Manunuzi ya Umma. Hatua hizi zinaonyesha ishara nzuri ya kuhakikisha kuwa watanzania wananufaika kutokana na Manunuzi ya umma kwani inakuza ajira na soko kwa bidhaa za ndani. Hivyo ufuatiliaji na utekelezaji unapaswa kufanywa ili kuhakikisha watanzania wananufaika kutokana na Manunuzi ya umma.