DMDP

Kuhusu Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project)

1. Utangulizi

Katika Mwaka wa fedha 2012/13 Serikali ilibuni Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) ikiwa ni kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi yenye dhamiri ya kupambana na changamoto kubwa nne; Kwanza kuondoa umaskini, pili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, tatu kupambana na rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na nne kudumisha Ulinzi na Usalama wa wananchi na mali zao.

Aidha, Mradi wa DMDP ni matokeo ya miradi miwili mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mradi wa wa kwanza ni ule ujulikanao kama Mradi wa uendelezaji wa miji minane kimkakati (Tanzania Strategic Cities Project – TSCP) unaotekelezwa katika Majiji ya Arusha, Mwanza na Mbeya na Manispaa za Kigoma Ujiji, Mtwara Mikindani, Dodoma, Kigoma Ujiji pamoja na Mamlaka ya Uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma – CDA. Mradi mwingine ni ule wa Uendelezaji Miji kumi na nane ujulikanao kama Urban Local Government Strengthening Programme (ULGSP). Kwa ujumla katika miradi hii miundombinu ya barabara, mitaro ya maji ya mvua, nyenzo muhimu za ukusanyaji na uhifadhi wa taka ngumu pamoja na mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika maeneo husika vimeboreshwa kwa kiwango kikubwa.

Katika mazingira ya hapa Dar es Salaam, Serikali iliamua kutekeleza mradi wa DMDP kwa kuiangalia Dar es Salaam katika hali ya upekee kutokana na kuwa:-

i) Jiji la Dar es Salaam linakua kwa kasi kwani inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030, Jiji hili litakuwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 10.

ii) Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutawala katika kuwajibika vyema kwa wananchi wake.

iii) Manispaa za Jiji zinahitaji nyenzo muhimu za ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa Serikali Kuu katika mipango na bajeti zake,

iv) Ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam unakabiliwa na makazi yasiyopimwa kwa kati ya asilimia 70 mpaka 80. Aidha, kutokana na ukuaji kasi wa Jiji la Dar es Salaam na mabadiliko ya tabia nchi yanayoikabili dunia, athari za mafuriko zinatarajiwa kuongezeka katika Jiji la Dar es Salaam. Hivyo, bila kuwa na mipango bora ya utoaji wa huduma, Jiji hili linaweza kutokukalika au kutotawaliwa.

2. Madhumuni ya Mradi wa DMDP

Madhumuni makubwa ya mradi wa DMDP ni kukabili changamoto zinazolikabili Jiji la Dar es Salaam kwa kutilia mkazo maeneo yafuatayo:-

i) Uboreshaji wa huduma za jamii kama miundombinu na kujenga uwezo wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam katika utoaji huduma,

ii) Kuchangia katika kukabili changamoto za mabadiliko ya tabia nchi,

iii) Kusaidia katika kukabili matukio makubwa ya dharura kama majanga ambayo yanaweza kulikabili Jiji la Dar es Salaam.

3. Maandalizi ya mradi wa DMDP

Sanifu mbalimbali zilifanywa kulingana na vipaumbele na upatikanaji na fedha. Baada ya usanifu kukamilika vipaumbele muhimu vilianishwa kwa kufuata vigezo muhimu bila kuangalia umaarufu wa maeneo au itikadi mbalimbali. Vigezo muhimu vilikuwa ni hivi vifuatavyo:-

i) Miradi inayounganisha maeneo ya watu wenye kipato kidogo na yaliyojengwa holela

ii) Miradi inayounganisha Wilaya na Mkoa

iii) Miradi inayounganisha maeneo mbalimbali na ukanda wa mabasi yaendayo haraka (BRT) ili kurahisisha usafirishaji

Vigezo hivyo viliibua miradi ifuatayo:-

i) Ujenzi barabara za mlisho (feeder roads) zenye urefu wa kilometa 65.6 katika Manispaa zote za Jiji ili kupunguza changamoto za msongamano;

ii) Ujenzi wa mitaro ya kutiririsha maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 31.8 katika maeneo ya mto Ng’ombe, Msimbazi, Gerezani Creek, Yombo na Kwashego ili kutatua changamoto za mafuriko

iii) Kupandisha hadhi makazi yaliyopangwa kiholela katika Kata 14 za Tandale, Mburahati, Mwananyamala, Gongo la Mboto, Kiwalani, Ukonga, Keko, Kilakala, Mbagalakuu, Mbagala, Mtoni, Yombo Vituka, Kijichi na Makangarawe kwa kujenga kilometa 145 kwa kiwango cha lami, kuweka nyenzo za ukusanyaji wa taka ngumu, kujenga mitaro ya kutiririsha maji ya mvua, kuweka taa za barabarani, kujenga njia za watembea kwa miguu, ujenzi wa maeneo ya mapumziko na vituo vya mabasi, ujenzi wa vyoo vya umma na ujenzi wa maeneo ya michezo.

iv) Kuandaa Mpango kabambe wa Mfumo wa Maji ya Mvua na Maji Taka (Storm Drainage and Sewerage Master plan) kwa kushirikiana na DAWASA/DAWASCO ambao utasaidia kupanua wigo wa mifumo kwa asilimia 100% kufikia 2030

v) Kundaa Mpango Mkakati wa kuendeleza Ukanda wa mabasi yaendayo haraka (BRT Corridor Development Strategy). Kwa kushirikisha Sekta Binafsi; kujenga masoko ya kisasa na ya kawaida, kujenga maduka makubwa (shopping malls) na ya kawaida, kuboresha maeneo ya utalii, kujenga maeneo maalum ya maegesho, kuweka njia za waendesha baiskeli na watembea kwa miguu n.k

vi) Kufunga mfumo wa kisasa wa ukusanyaji wa mapato katika Manispaa zote na kuepuka mianya ya kuvuja na ukwepaji wa kulipa kodi.

vii) Kujenga uwezo wa mwitikio wa haraka katika kukabiliana na majanga.

4. Hali ya Utekelezaji

i) Katika mwaka wa fedha 2015/16 Serikali iliingia Mkataba na Benki ya Dunia wenye thamani ya dola za Kimarekani 300 milioni za utekelezaji wa mradi wa DMDP kwa kipindi cha miaka mitano. Aidha, mfuko wa maendeleo ya nchi za Nordic (NDF) umechangia dola za Kimarekani 5 milioni kwa ajili ya kukabili changamoto za mabadiliko ya tabia Nchi na Serikali ya Tanzania ina changia dola za Kimarekani 25.3 milioni katika mradi huu.

ii) Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni zimeingia mikataba na Washauri kwa ajili ya usimamizi wa miradi itakayotekelezwa kwa kipindi chote cha miaka mitano.

iii) Katika mwaka fedha 2016/17 utekelezaji wa miradi ya DMDP utaanza kama ifuatavyo:-

Manispaa

Bajeti kwa Mwaka 2016/17 (Sh.)

Kazi zitakazoanza kutekelezwa

Temeke

72,804,468,467.00

  • Kujenga barabara za mlisho 14.51km
  • Ujenzi wa mitaro mikubwa 8.9km
  • Ujenzi wa barabara za mitaa 55km

Ilala

43,242,117,826.00

  • Kujenga barabara za mlisho 2.84km
  • Ujenzi wa mitaro mikubwa
  • Ujenzi wa barabara za mitaa 55km

Kinondoni

63,938,175,211.00

  • Kujenga barabara za mlisho 14.51km
  • Ujenzi wa mitaro mikubwa 8.9km
  • Ujenzi wa barabara za Mitaa 55km

Pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo katika ngazi ya Halmashauri za Manispaa, Sekretarieti ya Mkoa itakuwa na jukumu la ushiriki wa pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Manispaa katika maandalizi ya usimamizi wa utekelezaji wa mradi kupitia Sehemu ya Miundombinu.

Uongozi wa Mkoa unawaomba wananchi washiriki kikamilifu na watoe ushirikiano katika utekelezaji wa miradi itakayopita katika maeneo yao, kwani miradi hiyo ni kwa manufaa ya wananchi kwa ujumla lakini pia miradi hii italeta ajira kwa wananchi na itakuza uchumi wa wananchi katika maeneo hayo.

Aidha, kutekelezwa kwa miradi hii itaibadilisha sura ya Jiji la Dar es Salaam na kutoa muonekano ambao Mhe. Rais ameendelea kutilia msisitizo uwepo wa Miji nadhifu iliyopangwa na yenye mandhari nzuri, hivyo natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam miradi hiyo itakapokuwa inatekelezwa wailinde na kuitunza kwa maendeleo ya Taifa letu.

Soma Zaidi: http://www.dsm.go.tz/project-details/mradi-wa-uendelezaji-wa-jiji-la-dar-es-salaam-dar-es-salaam-metropolitan-development-project-dmdp