Kuhamisha Teknolojia
Sayansi na teknolojia ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya taifa lolote. Teknolojia ni kiungo muhimu katika miradi mbalimbali kama biashara na pia kwa maendeleo ya Taifa. Hakuna nchi ambayo inaweza kuendelea kiuchumi bila kufanya juhudi za kimkakati katika kutengeneza, kuratibu na kuhamisha teknolojia kutoka sehemu zingine za ulimwengu. kuhamisha teknolojia kumeonyesha mafanikio katika nchi mbali mbali duniani kama vile Malaysia, Singapore na Hong Kong. Ili uhamishaji wa teknolojia uweze kufanikiwa inapaswa kuigwa na kuenezwa kwa taifa linalohitaji. Uchunguzi uliofanywa juu ya uhamishaji wa teknolojia katika sekta ya ujenzi mwaka 2014 unaonyesha kuwauhamishaji wa teknolojia katika sekta hii ulikuwa mdogo kutokana na kutokuwa na mipango thabiti ya kujifunza kutoka kwa wenzetu wakati wa miradi mikubwa iliyogharimikiwa na serikali au wafadhili binafsi. Katika nchi kama vile Malaysia kuna mipango rasmi ya uhamishaji wa teknolojia ambao ni pamoja na makampuni ya nje kushirikiana na makampuni ya ndani wakati wa kutekeleza miradi na kumekuwa na mipango ya upendeleo kwa makampuni ambayo yameingia ubia na kampuni za ndani au kushirikiana nayo wakati wa mradi. Changamoto zinazoikabili uhamishaji wa teknolojia katika sekta ya ujenzi ni pamoja na ukosefu wa mpango mkakati, ukosefu wa fedha, uwezo mdogo wa makampuni za ndani.
Katika tasnia ya madini licha ya idadi ya uwekezaji wa moja kwa moja kuongezeka bado kumekuwa na ugumu wa kujua mafanikio kwa makampuni za madini za ndani katika kuongeza ujuzi katika teknolojia mpya. Sababu kubwa ya kukosekana kwa uhamishaji wa teknolojia ya kutosha ni uhusiano duni kati ya kampuni za nje na za ndani ambazo zinataka sera ziweze kuamua na kutoa mazingira ya uhusiano.
Uhamishaji wa teknolojia utaweza kuleta maendeleo nchini Tanzania kama sera, mikakati madhubuti na kuanzishwa kwa vyombo vya kusimamia utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na miradi ya ubunifu iliyolenga kukuza teknolojia. Hivi sasa kuna sera ya Sayansi na Teknolojia ya 1996 na Sera ya Utafiti na Maendeleo ya 2010 ambazo zinafanyiwa marekebisho.