Project Details

Imewekwa : 16-01-2019

Mradi wa EACOP

Project Description

Huu ni mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania

Mahali Tanzania
  • Key Figures

  • Employees
    6720
  • Status
    Inayoanza

Huu ni mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania. Mradi huu una urefu wa jumla ya kilomita 1443 kati ya hizo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1147 zipo Tanzania. Bomba linapita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Bomba vilevile linapita katika wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.

Matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni za kimataifa za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za TOTAL, TULLOW na CNOOC ulibaini uwepo wa mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5. Kutokana na ugunduzi huo imebainika uwezekano wa kuvuna mapipa kati ya bilioni 1.2 hadi 1.7. Kutokana na mahusiano ya ushirikiano ya muda mrefu na faida za kupitisha bomba nchini Tanzania Serikali ya Uganda na wawekezaji wa mkondo wa juu waliamua kujenga mradi huu kupitia Tanzania kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Lengo la Mradi

Lengo la mradi huu ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa katika soko la ndani na sehemu inayobaki kuuzwa nje kwenye soko la kimataifa kupitia bomba la mafuta.

Mikoa itakayopitiwa na Bomba la Mafuta Ghafi

Bomba la mafuta linapitia katika mikoa nane na wilaya ya 24 zaTanzania Bara ambayo ni (wilaya kwenye mabano):-

  • 1.Kagera (Bukoba Vijijini, Muleba na Biharamulo);
  • 2.Geita (Chato, Geita, Bukombe na Mbogwe);
  • 3.Shinyanga (Kahama Mjini);
  • 4.Tabora (Nzega Vijijini, Nzega Mjini na Igunga);
  • 5.Singida (Iramba, Mkalama na Singida Mjini);
  • 6.Dodoma (Kondoa na Chemba);
  • 7.Manyara (Hanang na Kiteto) na
  • 8.Tanga (Kilindi, Handeni Mji, Handeni Vijijini, Korogwe, Muheza na Tanga Mji).

Fursa

Mradi huu unatoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara katika hatua za awali za mradi (early works), wakati wa ujenzi (Construction) na wakati wa uendeshaji wa mradi (operations). Mradi pia unatoa fursa kwa watanzania kupitia makampuni ya watoa huduma kujiandikisha katika kanzi data ya EWURA ambaye ni mdhibiti wa mkondo wa chini na kati katika sekta ya uziduaji na vilevile kwa watanzania kujiandikisha kupitia kanzidata ya nguvukazi iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kupitia kitengo cha TaESA.

Hatua iliyofikia Mradi kwa sasa

Kwa sasa Mkataba wa mwisho kati ya Nchi za Tanzania na Uganda umeshasainiwa na ujenzi wa bomba la mafuta umekwisha anza na unategemea kukamilika ifikapo mwaka 2024.

Ardhi ya mradi imetengwa katika maeneo makuu matatu ambayo ni maeneo ya kipaumbele, eneo la bomba (mkuza) na sehemu ya matenki ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta. Mradi una fursa nyingi za kiuchumi na kijamii na unatarajia kuleta mabadiliko makubwa na manufaa kwa nchi zote mbili pamoja na wawekezaji. Mradi unatarajia kuzalisha ajira na kuwezesha jumla ya wananchi watakaonufaika na fursa zaidi ya 30,000 wakati wa ujenzi ukilinganisha na wakati wa shughuli za awali kabla ya ujenzi na wakati wa uendeshaji. Mradi wa Bomba utawezesha pia kutoa fursa mbalimbali za biashara zitakazotokana na mradi huu. Maeneo ya kipaumbele yatazingatia kambi za wafanyakazi (12), hifadhi za mabomba na kiwanda cha kuweka plastiki (1); eneo la mkuza litakuwa ni eneo litakapolazwa bomba pamoja na miundombinu mingine kama vituo vya kuongeza msukumo (4), kupunguza msukumo (2), vituo vya umeme n.k; sehemu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta – patakapojengwa matenki na jeti ya kupakia mafuta kwenye meli.

Gharama za kukamilisha ujenzi wa mradi wa bomba zinatarajia kufikia takribani Shilingi Trilioni 8 za Kitanzania. Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kwa maelezo zaidi kuhusu fursa za ajira na zabuni mbalimbali bonyeza links zifuatazo https://eacop.com/, http://eacop.com/jobs-tenders/

Kwa maelezo kuhusu kujiandikisha katika kanzidata ya watoa huduma bonyeza link ya EWURA kama ifuatavyo https://www.ewura.go.tz/na kupata maelezo kuhusu kanzidata ya nguvukazi bonyeza link ya TaESA http://taesa.go.tz/.